JUKWAA LA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA-na Peter Sarungi

Na Peter Sarungi (The next Speaker)

 Nitumie fursa hii kutoa shukurani kwa wote walio jitolea na hata kufuatilia kwa karibu juu ya uundwaji wa Jukwaa la Watu wenye Ulemavu Tanzania. Mpaka sasa tumekamilisha 95% ya taratibu za kusajili Taasisi hii muhimu kwa walemavu. Jamii ya watu wenye ulemavu imeendelea kutengwa katika mipango mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa sababu ya kukaa kimya bila kusema juu ya changamoto zetu, uwezo wetu, vikwazo tunavyokumbana navyo na hata mafanikio yetu. Ni muda sasa umefika wa kusema kwa nia ya kutetea na kushawishi maswala ya watu wenye ulemavu Tanzania ili na sisi Tanzania tufanane na wenzetu wa Afrika Mashariki walio amua kutekeleza kwa maneno na vitendo mkataba wa UN unao husu jamii ya walemavu na ni mkataba ambao Mh. Mkapa aliridhia na kusaini kisha Mh. Kikwete kuruhusu utungwaji wa sera na sheria no.9 ya watu wenye ulemavu na sasa kilichobaki ni kupiga kelele juu ya utekelezaji wake.

Ni jukumu letu sote kupiga kelele tena bila utengano na kwa sauti moja hata kama wewe sio mtu mwenye ulemavu lakini ukiguswa na hili basi ni sahihi kusema kwa nguvu hadi jamii, serikali na wadau wengine wapate kusikia ujumbe huu. Kuna msemo unasema hivi…

“Mtoto anayelia na kupiga kelele sana ndiye anaye pewa nyonyo na mama yake, ukinyamaza maana yake umeshiba”

Sidhani kama sisi watu wenye ulemavu tumeshiba katika nchi yetu, la hasha ila tuna ugulia kimya huku tukifa na tai shigoni. Ukimya wetu ndio unao tufunga, unao turudisha nyuma, unao tififisha ndoto zetu, unao tukosesha thamani na ndio sababu ya kutengwa na fursa.

Tanzania amka useme jambo kwa jamii hii ili na wewe ushiriki katika kutetea na kushawishi maswala ya watu wenye ulemavu Tanzania.

Leave a Reply