Kesha la asubuhi: Kufurahi katika neno

*Kesha la asubuhi*

_Jumanne Aprili 17, 2018_

*_Kufurahi Katika neno_* _Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi. Yeremia 15:16._

? Katika kutekeleza dini ya Biblia, kuna hitaji la subira, uungwana, kujikana nafsi na kujinyima. Lakini, kama Neno la Mungu litafanywa kuwa kanuni inayodumu maishani mwetu, kila linachotwambia inatupasa kufanya, kila neno, kila tendo lililo dogo, litadhihirisha kuwa sisi ni raia wa Yesu Kristo, kwamba hata mawazo yetu yamewekwa kwenye kifungo chake. Neno la Mungu likipokelewa moyoni, litaondoa nafsini hali ya kujitosheleza nafsi na kuitegemea nafsi.

? Maisha yetu yatakuwa nguvu kwa ajili ya kutenda mema, kwa sababu Roho Mtakatifu atajaza mioyo yetu kwa mambo ya Mungu. Dini ya Kristo itatekelezwa nasi; kwani nia zetu zipo katika upatanifu kamili na mapenzi ya Mungu. Baadhi ya wale wanaodai kuwa na dini ya kweli inasikitisha kwamba huwa wanapuuzia Kitabu kilicho Mwongozo utokao kwa Mungu ili kuelekeza kwenye njia ya mbinguni. Wanaweza kusoma Biblia, lakini kusoma tu Neno la Mungu, kama mtu asomaye maneno yaliyoandikwa kwa kalamu ya mwanadamu, kutampa mtu ujuzi wa juu juu tu.

? Kuuzungumza ukweli hakutatakasa wapokeaji. Wanaweza kudai kufanya kazi ya Mungu, wakati ambapo, kama Kristo angekuwa kati yao, sauti yake ingesikika, akisema, “Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Mathayo 22:29). Watu wa namna hiyo hawataweza kujua kile dini ya kweli inachokimaanisha.

? Kristo alisema, “Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” (Yohana 6:63). Yeremia anashuhudia juu ya Neno la Mungu akisema, “Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu.” Kuna uponyaji wa kimbingu katika Neno la Mungu, ambao wale waitwao wenye hekima na busara hawawezi kuupata, lakini ambao unadhihirishwa kwa watoto.

? “Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga” (Zaburi 119:130). Kama Neno hili litahifadhiwa moyoni, litakuwa ni hazina ya moyo, ambako vitatoka ndani yake vitu vipya na vya kale. Hatutaendelea kufurahia kufikiria mambo duni ya dunia, bali tutasema, “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu” (aya ya 105). – Review and Herald, Mei 4, Mei 4, 1897.

_TAFAKARI NJEMA MWANA WA MUNGU_

Leave a Reply