Kesha la asubuhi: Kuongozwa kwa Njia ya Ushuhuda Ulioandikwa

*Kesha la Asubuhi*

*Alhamisi, Tarehe 19/4/2018*

*Kuongozwa kwa Njia ya Ushuhuda Ulioandikwa*

▶Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi. Isaya 8:20.

▶Daima Roho Mtakatifu anaongoza kwenye Neno lililoandikwa na huwa anavuta usikivu katika suala la kiwango kikuu cha maadili cha uadilifu. Kuheshimiwa na Mungu kwa namna hiyo kwa kupata fursa hii ya pekee kushuhudia ukweli ni jambo la ajabu. Kristo aliwaambia wanafunzi wake mara kabla ya kupaa juu na wingu la malaika kumpokea na kumwondoa machoni pao, “Mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Matendo 1:8). Walifanywa wafae kumshuhudia Kristo kutokana na karama ya kimbingu ya Roho Mtakatifu.

▶Natamani kuwasisitizia ukweli kwamba wale ambao Yesu anakaa mioyoni mwao kwa imani kwa kweli wamempokea Roho Mtakatifu. Kila mtu anayempokea Yesu kama Mwokozi wake binafsi kwa uhakika pia anampokea Roho Mtakatifu kuwa Mshauri, Mtakasaji, Kiongozi na Shahidi wake. Kadiri muumini anavyotembea kwa karibu na Mungu, ndivyo ushuhuda wake unavyozidi kuwa wazi na kama matokeo yaliyo ya hakika, ndivyo mvuto wa ushuhuda wake utakavyokuwa wenye nguvu zaidi kwa wengine kuhusu upendo wa Mwokozi; ndivyo atakavyozidi kuonesha uthibitisho kwamba anathamini Neno la Mungu. Hiki ndicho chakula chake, ndicho kinywaji chake, kwa ajili ya kuridhisha nafsi iliyo na kiu. Anathamini fursa hii ya pekee ya kujifunza mapenzi ya Mungu kutoka katika Neno lake.

?Baadhi ya watu wanaodai kuwa waumini wameweka pembeni, wamegeukia mbali na Neno la Mungu. Wameipuuzia Biblia, Mwongozo ulio wa ajabu, kipimo cha kweli cha mawazo yote na wanadai kwamba wanaye Roho anayewafundisha, kwamba hili linafanya suala la kuchunguza Maandiko lisiwe la muhimu. Wote wa namna hii wanasikiliza hila za Shetani, kwani Roho na Neno wanakubaliana. Maandiko yanasema, “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” Yeye ambaye ukweli unamweka huru ndiye mtu ambaye yuko huru kweli. – Manuscript Releases, vol. 14, uk. 70, 71.

Leave a Reply