“NIMECHAGUA UKWELI KWENYE SIASA, SIO BARIDI WALA MOTO.” -Peter Sarungi

Peter Sarungi (The next Speaker)

Siasa safi zinahitaji kuwa na demokrasia ndani yake, kuwe na uhuru wa kutoa mawazo mbadala, kuwe na desturi ya kuvumiliana hasa pale mnapopingana mawazo na kuwe na tabia ya kutafuta na kusema ukweli hata kama ukweli huo utakuwa mchungu.

Mtindo wa vijana wengi wa sasa ni wa ajabu sana katika siasa. Mtindo ulio gubikwa na tabia za uongo, unafiki, fitina, wasaliti, ndumilakuwili, kujipendekeza, kutafuta sifa, kukurupuka, ushabiki, na unazi usiokuwa na tija kwa taifa. Tabia kama hizi zina fifisha ubunifu, uzalendo, umakini, ujasiri na umahiri kwa vijana katika uongozi na uwajibikaji.  Tumejenga jamii ya vijana walio gawanyika kihisia, itikadi, maneno na kwa matendo yao, waoga wa kutetea ukweli, wepesi wa kushindwa na uovu, walio tayari kusema vya kukaririshwa. Ndio maana kuna vijana walio tayari kukosoa jambo lolote kutoka upande wa pili hata kama ni jambo jema kwa taifa na wapo tayari kusifia jambo lolote la upande wao hata kama ni sumu kwa Taifa. Wameamua kuwa baridi ama moto.

Mimi nimekataa kuwa sehemu yao, kuwa mtumwa wa fikra zao, kutumika katika malengo yao. Nimeamua kuwa mfuasi wa ukweli na kwa fikra huru. Nahitaji Ukweli ili uniweke Huru, ukweli utakao tibu Taifa ili vizazi vijavyo vipate kufaidika na ukweli huu.

Unga kuchagua ukweli ili tujenge Taifa lenye kuheshimu ukweli.

Asanteni sana.

Leave a Reply