Simulizi ya maisha ya mzee O.O Igogo: Baada ya miaka zaidi ya 40 akutana tena na rafiki yake!

“Wilson Simon Mande, aliyekaa kati, leo kampigia simu Mzee OOI na kumjuza kwamba yupo jijini Dar, kitongoji cha Mgeni nani?? Kwa furaha na bashasha nimemuomba niende kukutana naye na ikiwezekana nimkaribishe chakula cha jioni kwetu Kibada.

Mzee Wilson, kaka yangu, rafiki wa kweli na Mfadhili aliyenipa ajira ya kudumu kwenye kampuni ya Kibo Paper Industries Ltd mwaka wa1975, akiwa Afisa Utumishi, nami nikiwa mchoovu asiye na ajira, na aliyekimbiwa na ndugu waliohamia kusikojulikana huko nyuma. Kwa mtonyo wa rafiki yangu Saidi Kikungo a.k.a mapersonality leo hii tumeonana tangia mwaka wa 1978 tulipoachana akiwa Kibo nami nikienda NECO LTD.

Namshukuru Mungu wetu kwa kuniwezesha walau nami nimuonyeshe furaha ya kumbukizi ya wema aliyonitendea miaka hiyo.” 》》》》 Hayo ni maneno yake mzee O.O Igogo mwenyewe siku ya leo 01 /13 / 2021.

WEMA HAUOZI

Vijana wa zamani, waliohitimu elimu ya msingi mwaka 1968 pamoja, wakutana huko Mbande. Mzee. John Wao Abila ( Kati) akipeana mkono na Mzee 0.O Igogo alipomtembelea nyumbani kwa mwanae jioni ya leo.

Historia ya maisha yao Mzee O.O Igogo, alipoteza ajira mnamo mwaka wa 1973, naye akalazimika kujikimu kwa kaka yake mmoja, huku akiendelea kusaka ajira. Baada ya miezi kadhaa siku moja alipotoka mahangaikoni Kunduchi ambapo siku hiyo hakufanikiwa kupata kibarua cha kusaidia mafundi ujenzi, ikambidi kutembea kwa miguu toka huko Kunduchi Beach, hadi Keko Machungwa kwenye maskani ya familia ya kaka yake. Kwa mshangao na butwaa kubwa, alikuta maskani ya kaka yapo holaa! Yaani familia hiyo wamehama nyumba na kwenda kusikojulikana bila ya kumwambia dogo O.O Igogo. Ilikuwa majira inayokaribia saa mbili usiku, hivyo dogo O.O Igogo aliyekimbiwa, naye hana hata senti moja ya kujikimu usiku huo wala kesho yake alijikuta akiangua kilio cha simanzi huku majirani walioambiwa kisa cha kutorokwa wakimcheka kwa kejeli.

Dogo O.O Igogo hakuwa na la kufanya zaidi ya kujiendea kwenye geto lake na kujibwaga kitandani na njaa yake ya kutwa na uchovu wa kutembea zaidi ya kilomita arobaini kwa mguu.

Kati kati ya usiku huo, alisikia hodi mlangoni kwake akiitwa jina na huyo rafikiye John Wao Abila, akamfungulia mlango. Rafiki yake kwa huruma akamweleza sikitiko lake kuhusu hao ndugu waliomkimbia. Hivyo alikuja kumuaomba waende naye nyumbani kwake kupata msosi. Dogo O.O Igogo hakusita, naye wakaongozana kwenda huko kwake. Tangia siku hiyo alikuwa mfadhili wake hadi alipopata ajira kwenye kiwanda cha Kibo Paper Industries Ltd. Rafiki yake alimpa funguo za mlango wake na kumruhusu kujipikia mchana na jioni iwapo yeye atakuwa yupo kazini.

Jana usiku nilimpigia simu ili nimjulie hali huko Utegi, naye akanijuza kwamba yupo hapa Dar. Hivyo ilinibidi kufunga safari na kumtafuta alipo huko Mbande ili nimjulie hali na kusaidiana panapo bidi. Wema wake na fadhali aliyonitendea ni hazina ya milele kwake, namshukuru siku zote, na iwapo pana mahala ana jambo la kumsaidia, siwezi kusita. NIMEFARIJIKA SANA KUMUONA LEO

*** Imeandikwa na Mzee 0.O Igogo November 26, 2020, nimeambatanisha na hiyo ya leo hapo juu kwasababu hii ya November26, 2020 nilikuwa sijaipost humu***

Leave a Reply