Simulizi za maisha ya mzee O.O Igogo kwa maneno yake mwenyewe!

Za asubuhi marafiki wapendwa. Natumai soote tumeamka salama na hao wadogo wasiyoweza kuwasiliana kwenye group. Jana ilikuwa siku yangu ya kumbukizi ya mambo ya ujanani, kama alivyosema Mama ni kweli niliwahi kushiriki kanywaji kati ya mwaka 1972 hadi 1979. Nilishuhudia matukio mengi ya kuchekesha na kuhuzunisha ndani ya kipindi hicho. Nakubaliana fika na Rais Mstaafu wa Nchi ya Merekani OBAMA, alichokiandika kwenye kitabu chake kilichompa Umaarufu kiitwacho THE DREAM FROM MY FATHER. Aliota njozi toka Baba yake, na wala siyo ndoto!!!Nami mwaka wa 1979, nikiwa kazini wilaya ya Geita enzi hizo, kwenye machimbo ya dhahabu Nyarugusu, nikiwa Msimamizi wa Ujenzi wa mitambo hapo mgodini na Shirika la NECO Ltd. Nilienda kijiji cha jirani kumtembelea Mama yangu mdogo, aitwaye Leokadia Ombwa Olwengo, mdogo wake Rhoda Nyolwengo. Yeye na Vijana wake walikuwa wachimbaji wadogo wadogo. Nilikuwa na gari la Shirika na ikawa shangwe ya hali ya juu nilipofika hapo kwake. Kuku wawili walipoteza uhai ghafla kuwa kitoweo rasmi. Mama alikuwa mtengenezaji maarufu wa pombe ya kienyeji iitwayo APELO, yaani CHANG’AA🙆🏻 Ile furaha ya kukutana na ndugu zangu, nao kuniona nimekuwa Bosi naendeshwa na gari la Shirika, ikazua unywaji wa kilevi Apelo bila kipimo. Nilivyorudi kambini na kuingia chumbani sikujuwa. Ila usiku huo wa tarehe 7/6/1979, nilijiwa njozini na Marehemu Baba yangu Mzee William Olung’a Igogo. Aliniita kwa sauti ya juu sana nami nikamuitikia, nilikuwa napepesuka kwa ulevi, manano aliyoniambia ni:- MBONA UNAHARIBIKA KWA POMBE?? ACHA ULEVI, UNAPOTEA!! ACHA KABISA👏

Asubuhi yake nilipoamka, nilikuwa hovyo, hovyo kweli, kweli!!! Nilijikuta nimelala kwenye matapishi yangu yanayonuka kama taka teke teke ya chooni. Mchovu kupindukia, kichwa kinawanga na kugonga kama nyundo!! Ilinilazimu kujifanyia usafi huku nikiitafakari hayo maneno ya njozini, niliyohaswa na Marehemu Baba!! Sikuweza kwenda kazini siku hiyo, ilipofika mchana nilipata mlo kwenye kantini ya hapo Camp, na hatimaye nikaamwambia dereva anipeleke Geita mjini, nilikwenda moja kwa moja kwenye duka la Vitabu, na kununua kijitabu kidogo cha Agano Jipya. Nikaanza kuisoma msitari kwa msitari, kurasa hadi kurasa ifuatayo hadi mwisho, na nikairudia mara kadhaa.Ni kweli tangia siku hiyo hadi leo hii, zaidi ya miaka arobaini sijaweka kinywaji cha aina yoyote kinywani mwangu. Naamini bila mashaka ya aina yeyote kwamba Maandiko matakatifu isemavyo kwamba Baba na Mama yako ndiyo Mungu wako wa Duniani, ni kweli haswaa.

Mzee Igogo na mjukuu wake Cecilia Chaulo

***imeandikwa na mzee O.O Igogo (muhusika) na kunukuliwa hapa na Alpha O.O Igogo (blogger)***

Leave a Reply