Kesha la asubuhi: CHUMVI YA DUNIA

                  KESHA LA ASUBUHI

                  Juma Pili 3/6/2018
  
             **CHUMVI YA DUNIA**“Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu” Mathayo 5:13

Mungu atatenda kazi pamoja na kanisa, lakini si bila ushirikiano wao. Hebu kila mmoja wenu aliyeonja Neno zuri la Mungu “nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16). Yesu anasema, “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.” Chumvi inayookoa, yaani mvuto wa Mkristo, ni upendo wa Yesu moyoni, ni haki ya Kristo inayotawala rohoni. Ikiwa yule anayedai kuwa mtu wa dini atatunza ufanisi wa imani yake unaookoa, imempasa kuiweka haki ya Kristo mbele yake daima, na kuwa na utukufu wa Bwana kama thawabu. Ndipo uweza wa Kristo utakapofunuliwa katika maisha na tabia.

Oh, tutakapofika kwenye malango ya dhahabu, na kuingia katika mji wa Mungu, je, kuna yeyote atakayeingia pale ambaye atajutia kwamba aliyatoa maisha yake kikamilifu kwa Kristo? Hebu sasa tumpende kwa upendo ulio kamili, na kushirikiana na viumbe wa mbinguni, ili tupate kuwa watendakazi pamoja na Mungu, na kwa kufanywa washirika wa tabia ya Uungu, tuweze kumdhihirisha Kristo kwa wengine. oh, laiti tungepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu! Laiti miale miangavu ya Jua la Haki ingeangaza katika vyumba vya mioyo yetu na akili zetu, ili kwamba kila sanamu iondolewe na kufukuzwa kutoka katika hekalu la moyo! Laiti ndimi zetu zingefunguliwa ili kuzungumzia wema wake, na kueleza juu ya uweza wake!

Kama ukiitikia kuvutwa na Kristo, 6hutashindwa kuwa na mvuto kwa mtu fulani kupitia uzuri na uweza wa neema ya Kristo. Hebu tumwangalie na kubadilishwa katika mfano wake Yeye ambaye ndani yake unakaa utimilifu wote wa Mungu kwa jinsi ya mwili, na kutambua kuwa tumekubalika katika huyo Mpendwa, “mmetimilika katika Yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka” (Wakolosai 2:10). – Bible Echo, Feb. 15, 1892.

Leave a Reply