Kesha la asubuhi: Roho Hatimaye Aondolewa

                   *Kesha la Asubuhi*

                          *Alhamisi*

                     *Tarehe 31/5/2018*

                     *Roho Hatimaye
                          Aondolewa*??Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Ufunuo 22:11.

??Wakati ujumbe wa malaika wa tatu utakapofungwa, rehema haitaendelea kusihi tena kwa ajili ya wakazi wa dunia wenye hatia. Watu wa Mungu wametimiza kazi yao. Wamepokea “mvua ya masika,” “kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana” (Matendo ya Mitume 3:19), na wako tayari kwa ajili ya saa ya majaribio iliyoko mbele yao. Malaika wanaharakisha kwenda mbele na kurudi nyuma kule mbinguni. Malaika mmoja anarudi kutoka duniani na kutangaza kuwa kazi imekwisha; jaribio la mwisho limeletwa juu ya dunia, na wote waliojithibitisha wenyewe kuwa ni waaminifu kwa sheria za Mungu wamepokea “muhuri ya Mungu aliye hai” (Ufunuo 7:2).

??Kisha Yesu anaacha kazi yake ya upatanisho katika patakatifu pa mbinguni. Anainua mikono na kwa sauti kuu anasema, “Imekwisha,” na jeshi lote la malaika wanaweka chini taji zao anapotoa tangazo makini: “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu: na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu: na mwenye haki na azidi kufanya haki: na mtakatifu na azidi kutakaswa.” (Ufunuo 22:11). Kila kesi imeamuliwa kwa ajili ya uzima au mauti. Kristo amefanya upatanisho kwa ajili ya watu wake na kufutilia mbali dhambi zao. Idadi ya watu wake imekamilishwa; “ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote” (Danieli 7:27), inakaribia kupewa kwa warithi wa wokovu, na Yesu atawale kama Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.

??Anapotoka katika patakatifu, giza linawafunika wakazi wa dunia. Katika wakati ule wa kuogofya watakatifu inabidi waishi mbele za Mungu aliye mtakatifu bila kuwa na Mwombezi. Kizuizi ambacho kimekuwapo juu ya waovu kinaondolewa, na Shetani anakuwa na mamlaka kamili juu ya wale ambao hatimaye hawakutubu. Uvumilivu wa Mungu umefika mwisho. Dunia imekataa rehema yake, imedharau upendo wake, na kuikanyaga chini ya miguu yao sheria yake. Waovu wamevuka mpaka wao wa rehema; Roho wa Mungu, akiwa ameendelea kupingwa, hatimaye sasa anaondolewa. - The Great Controversy, uk. 613, 614.

Leave a Reply