TANZANIA INAHITAJI MIFUMO IMARA KULIKO VIONGOZI IMARA- Peter Sarungi

Bara la Africa ni moja kati bara lililo wahi kutawaliwa na viongozi washupavu, majasiri na imara kwa muda mrefu bila mafanikio. Historia imeshuhudia viongozi jasiri na imara kama Mandela, Kwame Nkuruma, Gadafi, Idd Amini, Nyerere, Samwel Doo, Samora, Patrick Lumumba, Mugabe, Kawawa Simba wa vita, Mobutu Seseko, Savimbi, Karume, Kabila sr, Kenyatta sr, Obotte, Kagame, Satta na wengine wengi ambao walitikisa Afrika wakati wa utawala wao na wengine wapo mpaka sasa. Historia inaonesha kuwa watawala hawa walikuwa Imara ingawa wengine walitawala kwa mabavu, vita, mauaji ya alaiki na wengi walitawala nje ya mfumo wa demokrasia kupitia chama kimoja. Pamoja na uimara na ujasiri wa hawa viongozi bado Afrika imeendelea kulia na kuteseka na umasikini, maradhi na ujinga kwa viongozi na wananchi wao, Bado Afrika imeendelea kumwaga damu yao wenyewe kwa wenyewe, Bado Afrika imeendelea kuwa dhaifu kutokana na utengano dhidi ya mataifa ya magharibi na Asia, Bado Afrika imeendelea kuwa tegemezi katika afya, elimu, teknolojia, biashara, uchumi, utawala na mengi ambayo yanatoka nje ya afrika.

Tanzania tumebahatika kupata kiongozi imara, shupavu, jasiri na mwenye msimamo. Kiongozi anayeweza kufanya maamuzi na akasimamia maamuzi yake bila kutetereka hata kama yatakuwa na makosa, kiongozi anayethubutu kupita viongozi watatu waliopita. Huyu ni Dr John Pombe Magufuli (Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), Mimi binafsi namkubali sana Mhe. JPM ingawa ana baadhi ya mapungufu kama binadamu lakini bado ameonesha kuwa yeye ni imara. JPM kwa sasa amekuwa ni gumzo kwa bara letu la Afrika na dunia kwa ujumla. Nimepata kuona taarifa nyingi sana kutoka nchi zingine Afrika na Duniani kuhusu uimara wa JPM na hata mwaka uliopita JPM amekuwa ni Raisi wa Afrika aliyejadiliwa na kupata umaarufu mkubwa kuliko maraisi wengine. Hii ni tunu na sifa nzuri kwa utawala wake.

Pamoja Uimara wa JPM, Bado Tanzania tumendelea kulia kilio cha uchumi duni, afya mbovu, elimu duni, demokrasia na udikteta, uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa haki mahakamani, utawala bora, utumiaji wa nguvu na vitisho, wajibu wa bunge na wabunge, uelewa wa haki na wajibu wa raia, uchaguzi huru na wa haki, uzalendo na utaifa. Haya ni mambo yanayo endelea kurudisha nyuma maendelea ya taifa letu kwa kasi kubwa sana.

Hii ina sababishwa na Mifumo mibovu, kandamizi na yenye mianya ya kutenda maovu. Mifumo inatoa nguvu nyingi kwa kiongozi mmoja bila kuwa na njia za kudhibiti akikosea, mifumo inayo elekeza kiongozi kuwa juu ya sheria kwa kauli na matendo, mifumo inayo weza kuyumbishwa mda wowote bila kujali athari, mifumo inayo unganisha chama na serikali kuwa kitu kimoja, Mifumo tegemezi katika taasisi za nchi.

Hii mifumo mibovu ndio chanzo cha wana nchi kuendelea kulia vilia vilivyo zoeleka. Kwa aina ya mifumo hii, hata aje malaika kutoka mbinguni kuja kutawala bila kubadili ni sawa na kutwanga maji ndani ya kinu. Tunaweza kuwa viongozi imara kam JPM hata 50 lakini kwa mifumo yetu bado tutaendelea kuumia kila siku.

Peter Sarungi a.k.a The Next Speaker-Baba Pilato!

#MyTake

Bora kuwa na Mifumo imara itakayo weza kulinda maslahi ya nchi na wananchi wake hata kama kiongozi wa mfumo atakuwa legelege, bado mfumo utamnyoosha na kumlinda kuliko kuwa na kiongozi imara ndani ya mifumo dhaifu, maana siku kiongozi imara akibadilika basi nchi itarudi nyuma tena.

Mhe. JPM ni kiongozi Imara lakini mifumo ya serikali na taasisi zake bado zinaonesha udhaifu mkubwa na ndio maana utumbuaji ni mkubwa mno, Yaani kila kiongozi anayeguswa katika taasisi ni kama ameoza kwa rushwa, uzembe, uvivu na mengine mengi.

Tunahitaji mifumo imara kama ya jirani zetu Kenya na Zambia wanaoweza kusimamia matakwa ya wana nchi kisheria bila kutetereka.

Leave a Reply