Kesha la asubuhi: Kwa Mioyo Minyenyekevu

*Kesha la asubuhi*

_Kwa Mioyo Minyenyekevu_

*Jumanne Aprili 10, 2018*

Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu. Isaya 57:15.

? Wale wote watakaolijia Neno la Mungu ili kupata mwongozo, wakiwa na akili za unyenyekevu zenye kupenda kujua, wakidhamiria kujua masharti ya wokovu, wataelewa kile yanachosema Maandiko. Lakini wale wanaokuja katika uchunguzi wa Neno wakiwa na roho isiyokubaliwa nalo, watachukua kwenye uchunguzi mwelekeo ambao uchunguzi huo haukuuweka. Bwana hatanena na akili ambayo haijali. Huwa hapotezi maelekezo yake kwa mtu ambaye kwa kukusudia kabisa hana kicho na amechafuka. 

? Lakini mjaribu huwa anaelekeza kila akili inayokubaliana na mapendekezo yake, naye yuko tayari kuifanya sheria takatifu ya Mungu kuwa kama vile haina maana. Inatupasa kunyenyekeza mioyo yetu, tena kwa uaminifu na kicho tuchunguze Neno la uzima; kwani moyo ulio mnyenyekevu na wenye toba ambao ndio tu uwezao kuiona nuru. Akili, moyo, nafsi, ni lazima viandaliwe kuipokea nuru. Ni lazima pawepo ukimya moyoni. Ni lazima mawazo yasalimishwe na kuwekwa kwenye kifungo cha Yesu Kristo. 

? Hali ya kujivunia ujuaji ya nafsi na kujitosheleza nafsi lazima vikemewe mbele za Neno la Mungu. Bwana huwa ananena na moyo unaojinyenyekeza mbele zake. Kwenye madhabahu ya sala, kiti cha enzi cha neema kinapoguswa kwa imani, huwa tunapokea mwenge wa kimbingu kutoka mkononi mwa Mungu unaoangazia giza letu na kutusadikisha juu ya umuhimu wetu kiroho. 

? Roho Mtakatifu huchukua mambo ya Mungu na kumfunulia yeye aliye mwaminifu katika kuitafuta hazina ya kimbingu. Tukikubali uongozi wake, yeye hutuongoza kwenye nuru yote. Tunapotazama utukufu wa Kristo, tunabadilishwa na kufanana naye. Tunakuwa na ile imani inayotenda kazi kutokana na upendo na kusafisha moyo. Mioyo yetu hufanywa upya tena, nasi tunafanywa kuwa tayari kumtii Mungu katika mambo yote. –Review and Herald.

*MUNGU AKUBARIKI MWANA WA MFALME*

Leave a Reply