Kesha la asubuhi: Mwenye Wazazi Wanaojali

            *KESHA LA ASUBUHI*

          _JUMATATU MEI 07, 2018_

        *Mwenye Wazazi Wanaojali*  _Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usini-ondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. Zaburi 51:11-13._

?Ni ombi la namna gani hili! Ni dhahiri kiasi gani kuwa wenye dhambi walioko nyumbani hawapaswi kutendewa kwa kutokujali, bali kwamba Bwana anawaangalia kama walionunuliwa kwa damu yake. Katika kila kaya ambamo ndani yake wamo ambao hawajaongoka, inapaswa kuwa kazi ya wale ambao wanamjua Bwana kutenda kwa hekima kwa ajili ya wongofu wao. Bwana kwa hakika atabariki juhudi za wazazi, wakati ambapo kwa kicho na upendo watajitahidi kuokoa roho za walio katika kaya zao. Bwana Yesu anasubiri kuonesha neema.

? Kwamba kazi ingelianza moyoni! “Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.” (Zaburi 51:16, 17). Basi hebu na ifahamike na wanakaya wote kwamba kazi hii lazima ianze moyoni. Moyo lazima utiishwe na kufanywa kuwa na toba kupitia katika uwezo wa Roho Mtakatifu unaoumba, na kufufua. Kwa kutambua msaada wa wakala huyu mwenye nguvu, je wazazi hawawezi kufanya kazi kwa ari na upendo zaidi kwa ajili ya wongofu wa watoto wao kuliko walivyowahi kufanya hapo nyuma?

?Ahadi ya Bwana ni kwamba “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.” (Ezekieli 36:25-27).

? Roho wa Bwana anapofanya kazi katika mioyo ya wazazi, maombi na machozi yao yatakuja mbele za Mungu, watasihi kwa bidii, na watapokea neema na hekima kutoka mbinguni, na watakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ajili ya watoto wao ambao hawajaongoka. Kadiri Roho huyu anapodhihirishwa nyumbani, ataletwa kanisani, na wale ambao ni wamisionari wa nyumbani nao pia watakuwa mawakala wa Mungu kanisani na katika dunia. Taasisi ambazo Mungu amezipandikiza zitabeba tabia tofauti kabisa. - Review and Herald, March 14, 1893.

*TAFAKARI NJEMA NA MUNGU AKUBARIKI MTOTO WA MFALME*

Leave a Reply