“USHABIKI WA VYAMA VYA SIASA NI TOFAUTI NA USHABIKI WA VILABU VYA MICHEZO.” – Peter Sarungi

FB_IMG_1471977078685Na Peter Sarungi (Next Speaker)

Nakumbuka tangu nilipoanza kufuatilia mchezo wa mpira wa miguu nikiwa darasa la kwanza katika shule ya walemavu (Salvation Army) sijawahi kuhama Yanga pale nilijikuta nafurahia timu ya Yanga chini ya wacheza nyota kipindi hicho kama lunyamila, chambua, mohamed machinga na wengine wengi. Desturi ya ushabiki wa vilabu vya michezo katka historia ya soka inaonesha kuwepo kwa uvumulivu wa hali ya juu kutoka kwa mashabiki wa vilabu hasa pale wanapo boronga au hata kushuka daraja (mfano kwa sasa Arsenal na Liverpool). Mashabiki hushangilia timu husika iwe kwa shida ama kwa raha yaani wafungwe ama washinde bado ataendelea kuwa mshabiki wa timu husika. Hivyo ushabiki wa vilabu una lengo moja la kupata burudani pale timu inaposhinda.

Kwenye siasa hali iko tofauti kabisa. Siasa inagusa maisha ya kila siku ya mwananchi katika nchi. Siasa inawagusa watoto, vijana, wazee, wakulima, wavuvi, wachimba migodi, wafanyakazi, wafanyabiashara, walimu, masikini, matajiri, wanasiasa na makundi yote katika jamii. Kila mwananchi na kila jamii inaguswa na maamuzi ya kisiasa katika nchi kwa namna fulani yaani kila unachokifanya kinawezekana kwa sababu ya mazingira ya kisiasa. Lengo la siasa sio kupata burudani kama ilivyo kwa timu za michezo bali ni kuboresha maisha ya kila siku ya mwananchi.

Kwa utafiti wangu nimegundua watanzania wengi wanafananisha ushabiki wa vilabu nya michezo na ushabiki wa vyama vya siasa. Hali hii ni hatari sana kwa ustawi wa siasa na demokrasia katika nchi. Mara nyingi unamkuta mtu ana kuwa mfuasi wa chama cha siasa mpaka anapata upofu wa fikra yaani hata kama chama chake kinaboronga katika kuboresha maisha yake bado atakuwa mkaidi na mwenye kutetea chama. Hii hali imefanya watu wasomi na wenye heshima zao kuweka usomi wao mfukoni ili kutetea maslahi ya chama, hata haki ya kuhamia chama fulani inakuwa ni fedhea kwa mtu mpaka anaitwa majina mengi kama msaliti, mroho, malaya wa siasa. Yaani unapohama ni shida na unapohamia napo shida ipo, huu ni ushabiki wa Vilabu vya mpira, sio wa vyama vya siasa. Aina hii ya ushabiki wa vilabu katika siasa ndio sababu ya kuwepo kwa uadui kwa mashabiki na unagawa taifa kwa majina ya kejeli kama vile ndugu yangu Magoiga SN anavyowaita upande wa pili NYUMBU na Ben sanane anvyowaita upande wa pili FISIEMU. Ushabiki huu ndio sababu ya kupata baadhi ya wabunge ambao hawana sifa, uwezo wala weledi ya kuwa viongozi lakini wanachaguliwa kwa sababu ya ushabiki huu wa ovyo kabisa.

#Mytake. Unapokuwa mfuasi wa chama fulani ni vizuri ukaangalia maslahi yako na ya wapendwa wako kama yanapatikana kabla ya kutetea maslahi ya chama lakini vilevile tusishangae tunapo mwona mwanasiasa anahama kutoka chama kimoja na kwenda kingine jua anatafuta falsafa inayomfaa. Tusitukanane wala kuitana majina ya ajabu kwa kwenda upande fulani.

Asanteni sana

Leave a Reply