Je wewe ni “Nyumbu?”

Hii nimeipata  mahala fulani nikaona ni share nanyi kwani kunaujumbe fulani kama ukiondoa mtazamo wa kisasa ukaangalia katika maisha yako ya kawaida utaelewa vizuri huu ujumbe. Soma mwenyewe….. FB_IMG_1447084101361“By kababu:

Mafuriko yameelekezwa baharini! Upinzani umefanya makosa mengi ya msingi na wengi wameshaandika haya – kuna kupokea makapi, kuna kuweka mayai yote kapu moja (kuachiana), kuna kushindwa kutangaza sera hata siku ya ufunguzi wa kampeni, kuna kudhulumiana ndani ya ushirika, kuna kutowafikia wananchi wengi vijijini kwa kupenda starehe na misifa ya helikopta, kuna kutokujibu tuhuma nzito dhidi ya afya ya mgombea wao, kuna kutojibu tuhuma kuhusu chama kikuu ndani ya Ukawa kununuliwa, kuna kudharau mpinzani wao mkuu kana kwamba kazeeka au kachoka sana, kuna kudharau umuhimu wa watumbuizaji katika jamii ya kiafrika na kuwaita fiesta, n.k. Makosa ni mengi mno. Ila hii ilitokana na nini? UNYUMBU!

Nyumbu inasadikika ndiye mnyama mwenye IQ (ufahamu) mdogo kuliko wanyama wengi mbugani. Ni mnyama ambaye mwindaji hasumbui akili yake sana japo nyumbu ana maguvu na mapembe makali! Kichwani hamna kitu! Nyumbu hujihami kwa kuotea! Huota kuwa simba au mwindaji mwingine yeyote akija atamla jirani yake na si yeye! Kwa hiyo aendapo nyumbu mwenzie na yeye huenda! Nyumbu mwenzie akipiga kona na yeye hupiga kona! Nyumbu mwenzie akisimama na yeye husimama! Nyumbu mwenzie akiruka na yeyehakawii!

Ndio maana katika lile ajabu mojawapo la dunia litokealo mtoMara kule Serengeti mamba hujilia nyumbu hadi wanakinai! Akitokea nyumbu mmoja akaruka mtoni au akamsukuma mwenzie basi nyumbu wote watarukia mtoni au watasukumana hadi wadumbukie mtoni.

Tabia hii ya nyumbu tumeiona katika kampeni za Ukawa! Wenyewe kwa vinywa vyao tumewasikia wakijinadi ALIPO NA SISI TUPO! Yaani hata akitumbukia mtoni na wao watajiloweka humo! Hata pale ilipokuwa dhahiri kipenzi chao ni mgonjwa taabani tumewasikia wakisema TUTAMPA KURA HUYOHUYO HATA KWA MACHELA TUTAMPELEKA IKULU! Ni unyumbu ulikuwa upo kazini! Ndioo! Nyumbu hawanamuda wa kufikiri hata kidogo! Husukumana na huigana matendo! 

Ni katika unyumbu huu watu walishindwa kufanya tafakuri yakina! Hata pale nyumbu mkuu aliposema atawaachia watu waliohukumiwa na mahakama ya juu kabisa nchini kwa makosa mazito kabisa bado nyumbu wadogo walirukaruka kushangilia!Si nyumbu? Hata pale wawindaji walipotuhumu kuwa nyumbu mkubwa nimgonjwa badala ya kuweka mkakati wa kuwaaminisha wapigakura kuwa nyumbu mkuu yuko ngangari wao ndio kwanza wanasema TUNATAKA HUYO HUYO MGONJWA! 

Tabia hii ya unyumbu imesababisha anguko kuu nililolitabiri liwe kweli! Hili ni anguko kuu kwa kuwa hakika mwaka 2020 watu watasita kugeuka nyumbu! Bahati mbaya sana barani Afrika ili upinzani uweze kushika dola unyumbu unahitajika.  Kwa kawaida huwa anatokea almaarufu (celebrity) ambaye anatengeneza manyumbu wengi! Huyu Almaarufu akijua kucheza politics of wildbeasts anawashangaza watawala. Akishindwa huwa anatoweka kama alivyochomoza! Ni kwa kuwa kwa bahati mbaya zaidi unyumbu haujirudii! Ukipita umepita.”FB_IMG_1447084057928Kama nilivyo sema hapo juu kuwa tuondoe huu ujumbe kwenye mazingira ya kisiasa na kuweka mazingira ya maisha yetu ya kawaida. Je wewe ni “Nyumbu?” Wewe ni wale watu ambao wanashabikia vitu bila hata kujua ukweli  au  undani wa jambo? Je wewe ni mmoja wa watu ambao wanashabikia ugomvi na kusambaza chuki juu ya mtu fulani kwasababu tuu rafiki yako au mtu fulani kasema au mtu fulani naye yupo kwenye hilo group basi nawe unafuata tuu bila kufanya uchunguzi wowote? Je wewe ni “Nyumbu” wa kuiga style fulani ya maisha just because so and so are living that life style? Binadamu wakaida mwenye akili zake zote timamu huwa lazima anamisimmo yake au muongozo yake inayo ongoza maisha yake. Sio kufanya ushabiki tuu wa kufuata mkumbo! Siyo kila kitu kizuri ni kwaajili yako au kinakufaa vingine unatazama halafu unageuza shingo upande wa pili na kuendelea na maisha yako! Acha ushabiki usio na tija! Acha kuwa “Nyumbu!”

Leave a Reply