Watanzania yatupasa kubadilika – Sehemu ya kwanza: (MIAKA 10 ILIYOPITA)

Peter Sarungi
Peter Sarungi

Miaka mitatu nyuma watanzania wengi walijikuta wakiwa katika hali ya kukata tamaa baada ya mifumo mingi ya serikali na uendeshaji wake kutokidhi mahitaji ya watanzania ki uchumi, siasa na jamii.

Mimi nilikuwa mmoja wapo niliyekuwa naumia sana nilipokuwa nikipata taarifa za utendaji wa serikali na vitengo vyake kama polisi, mahakama, ardhi, afya, elimu, uchumi na mbaya zaidi ni taarifa za ufisadi wa nchi. Ilifika mahala ufisadi ukawa ni wimbo ulioimbwa na kila mwananchi kwa kusifia au kulalamikiwa.

kusifika kwa ufisadi na rushwa kulianza kuota mizizi kwa watanzania hasa vijana waliokuwa wakichipukia katika kazi na kupewa vitengo either kwa kushikwa mkono na mnene flani au kwa juhudi zake. Vijana tulikuwa msemo; Ukipata kitengo serikalini itumie vilivyo kutusua maana nchi haina mwenyewe. Vijana wengi walikosa uzalendo na uchungu wa nchi kutokana na tabia waliyoikuta kutoka kwa viongozi wao ambao walikuwa wakiitafuna nchi bila huruma. Vijana walifanya kufuru kwa kujenga majumba makubwa na magari ya kifahari ndani ya mda mfupi (Miezi 6) akiwa katika kitengo, Tabia hii ilisababishwa na wanasiasa waliotumia pesa nyingi kupata madaraka na uongozi na pindi walipopata uongozi waliwashawishi watendaji kufanya mambo yasiyokuwa ya kizalendo kwa nchi ili kurudisha garama na kupata faida zaidi na hata mtaji wa kuwekeza katika uchaguzi ujao.

Jamii zetu ziliathirika sana na tabia hii hasa vijana wetu wa kike maana ilifika mahala vijana wa kike wakaishi maisha ya kuigiza badala ya kuishi ualisia wao, wengi wao waliishi maisha ya kifahari pasipo kufanya kazi, mapenzi ya kweli yakawa ni historia, ndoa zikawa ni kwaajili ya kutoa nuksi kisha zinavunjika, kubeba mimba na kupata mtoto mmoja ikawa ni fashion na swaga za mabinti. Vijana wengi wa kiume mijini nao hawakupenda kufanya kazi za kuumiza akili, hawakupenda kufanya kazi kwa utaratibu na hawakuwa na uvumilivu katika maisha. Kila kijana alitamani akishapata kazi tu aweze kumikili gari, nyumba na mtoto mkali baada ya mda mfupi maana kwa kipindi hicho pesa iliweza kununua hadi mapenzi kutoka kwa baadhi ya mabinti waliojiona wazuri saana. Hivyo vijana wengi wakajiingiza katika ajira za kisanii na zingine zisizo halali kama utapeli, udalali waliolazimisha mifumuko ya bei, wauza poda, wafanyakazi hewa, mafisadi serikalini na wengine wakenda kwa wanganga na kutoa kafara za kutisha ili tu apate pesa ya kutamba na kufanya kufuru mitaani.

Siasa za nchi nazo zilibadilika sana kwa viongozi wetu ndani ya miaka 10 iliyopita. Viongozi walituaminisha kuwa kama huna cash basi siasa haikufai na hata wapiga kura tuliaminishwa kuwa mpigie kura anayekupa cash yaani kura zetu tuliziuza kwa pesa na zawadi mbalimbali. Siasa zikawa ni za maji taka kila mwanasiasa anatafuta pesa na umaarufu wa kuhonga ili aendelee kuchaguliwa. Wananchi hatukuona tena umuhimu wa siasa ikiwa viongozi tunao wachagua hawakidhi wala kutekeleza ahadi zao kwa jamii na wanasiasa safi walinyimwa kura kwa sababu ya kukosa cash na badala yake wafanya biashara na matajiri wa mitaa na majimbo ndio walioshindana kununua kura. Hali hii ilififisha dhana ya uchaguzi na demokrasia katika siasa.

Uchumi wa nchi ndani ya miaka 10 nao uli athirika kutokana na tabia ya ufisadi. Nchi ilisomeka kukua ki uchumi katika makaratasi lakini wananchi wengi walikuwa ni mafukara mifukoni waliokuwa wakiishi kwa mlo mmoja kwa siku. Vyanzo vikuu vya uchumi vili binafsishwa na kumilikiwa na wafanyabiashara na wanasiasa wachache(20%) waliomiliki sehemu kubwa ya utajiri wa nchi(80%) wakati wananchi wengi masikini (80%) walimiliki sehemu ndogo ya utajiri(20%). Maamuzi mengi ya uchumi wa nchi yaliumiza sana wananchi masikini mfano bei za bidhaa muhimu na garama za usafirishaji wake, viwango vikubwa vya kodi na kodi zisizokuwa na ulazima, maamuzi ya kuagiza bidhaa au kutengeneza bidhaa pamoja maamuzi ya kuacha sekta binafsi kutawala uchumi. Ndani ya miaka 10 tumeona hazina za nchi zikiachiwa huru kwa wageni kuvunwa kwa malipo madogo serikalini na viongozi wachache walioingia mikataba mibovu pasipo kuweka mbele uzalendo na maslahi ya nchi. Tulipofikia ilikuwa ni Hatariii kwa vizazi vijavyo..

Itaendelea….

By. Peter Sarungi

Leave a Reply