Mahojiano maalum: Zawadi Kakoschke

Naomba utueleze Historia yako kwa ufupi:FB_IMG_1446687026185Naitwa Zawadi Owitti Kakoschke. Mama wa watoto wawili Amani na Malaika na mke wa Bart Kakoschke. Nimezaliwa miaka 39 iliyopita huko Songea, Tanzania. Ni mtoto wa pili wa marehemu Fatuma ambae anatokea mkoani Iringa.

Zawadi na baba yake mzazi; mzee Owitti.
                                                 Zawadi na baba yake mzazi; mzee Owitti.

Mimi ni mjaluo baba yangu anatokea Shirati Rorya mkoani Mara. Kwa sasa makazi yangu yako kwenye nchi za kiarabu ambapo mume wangu anafanyia kazi. DSCN7873Wewe ni mmiliki wa blog ya maisafari.com, ambayo hata mimi ni shabiki mkubwa sana wa blog yako. Je nini haswa kilipelekea wewe kuanzisha blog yako? FB_IMG_1446687035620Nilitaka kuhamasisha watanzania wenzangu kupenda mambo ya utalii na kwa kiasi kikubwa nimefanikiwa kwa hilo. Nitatoa mfano nchi yetu ya Tanzania ina vivutio vingi sana lakini sababu hatuna utamaduni wa kupenda utalii watu wengi hawajaribu hata kwenda kuangalia ni kitu gani haswa kinawafanya watu watoke nchi mbali mbali kuja kutembelea nchi yetu. Mimi kama mtanzania ambae napenda sana mambo ya utalii nikaona kuna haja ya kuwahamasisha watanzania wenzangu kwa njia ya blog ambapo huwa naweka picha na maelezo mbali mbali ya nchi ambazo nimefanikiwa kutembelea.  FB_IMG_1446686789165Kusafiri ni moja ya mambo ambayo unapenda sana, unaweza kutuambia mpaka sasa umesha safari inchi ngapi duniani? Na inchi gani ambayo ungependa kufika lakini bado haujafika? Mpaka sasa nimebarikiwa kutembelea nchi kama thelathini na tano na miji mingi zaidi. Nchi ambazo nimefanikiwa kuzitembelea ni Tanzania, Kenya, Oman, Italy, Thailand, Cambodia, Australia, Singapore, Hongkong, Malaysia, UAE, England, France, Iceland, Switzerland, Qatar, Spain, Vatican City, America, Mexico, Cayman Island, Bahama, Jamaica, Colombia, Panama, Aruba, Portugal, St. Maarten, Malta, Us Virgin Island, Bonaire, Puerto Rico, Sri Lanka, Maldives and Holland, n.k. FB_IMG_1446686730179-1Zawadi, kusafiri kunahita fedha za ziada, je waweza kutueleza ni jinsi gani unaweza kumudu safari zako, nini haswa chanzo cha mapato yako kama utapenda kutuambia? Utalii unafanya kutokana na uwezo wako na si lazima uwe na pesa nyingi ndio uweze kutalii. Mimi kabla sijapata nafasi ya kutembelea nchi mbali mbali nilianza na utalii wa ndani kwanza ambapo nilifanikiwa kutembelea karibu mikoa yote ya Tanzania. Cha muhimu ni kujipanga tu kama vile unavyoweza jipanga kwa mambo mengine. Sisi huwa tunadunduliza kidogo kidogo mpaka pale tunapata pesa za kutosha na kuzitumia kwa ajili ya safari. Mimi na mume wangu tunapenda sana kusafiri kwa hiyo hatujisikii vibaya kutumia hizo pesa kwa ajili hiyo. Tunaamini pesa tunazotumia kwenye utalii hazipotea bure bali tunapata faida zaidi. FB_IMG_1446686604048-1Historia yako inaonyesha wewe ni dada wa Kitanzania ambaye umeolewa na mtu mwenye asili ya kizungu, je ilitokea tuu au ulikuwa na ndoto za kuolewa na mzungu siku zote? Nilikutana na mume wangu ambae anatokea Australia mwishoni mwa mwaka 2001 na mwanzo wa mwaka 2002 tulianza kuishi pamoja. Miaka miwili baadae tulifunga ndoa huko Sydney, Australia. Kusema ukweli siku ya harusi yangu ilikua ni siku ya furaha ya ajabu kwa sababu ndoto yangu imekua kweli.

Zawadi siku ya harusi yake
                                                 Zawadi siku ya harusi yake

Nimekua na ndoto ya kuolewa na hawa wenzetu toka nikiwa mdogo, nina sababu nyingi lakini kubwa sikutaka kuolewa na kuishi maisha ambayo mama yangu alikua anaishi ya UKE WENZA. Niliona kama nikitaka maisha ya ndoa yenye furaha basi ni mzungu tu ambae anaweza nipa hayo maisha ingawa kipindi hicho ilikua nayaona hayo maisha kwenye movie tu ha ha haaaa. Kitu kingine niliona wenzetu wazungu wamejifunza kuwa wakweli nami napenda sana watu wakweli. DSCN7906Unawatoto wazuri sana Amani na Malaika. Ilikuwaje ukawapa hayo majina ikizingatiwa umeolewa na “mzungu” wengi wangetarajia majina ya watu wenye asili hiyo? Asante, watoto ni zawadi kubwa namshukuru mungu kila siku. Nilitaka kuwaachia watoto wangu kumbukumbu ya nchi yangu Tanzania. Nilikua najua kila mara majina yao yatakapokuwa yanatamkwa lazima watu watakua wanauliza asili yake na hapo ndio habari ya mama yao inakuja katika picha. Namshukuru mume wangu alikubali kuwapa watoto wetu majina ya kwetu. FB_IMG_1442849273617Je, unawafundisha watoto wako Kiswahili na natamaduni zingine za Kiafrica haswa Tanzania? Pili huwa unapika vyakula vya kiafrika kwa familia yako? Ni chakula gani cha kiafrika ambacho wanapenda? Nasikitika kusema nimefeli kidogo katika suala la kiswahili mpaka sasa bado hawajui. Ni kosa langu mimi mama yao sikulichukulia kwa nguvu zaidi ambapo sasa ndio naona makosa yangu maana jinsi wanavyokua ndio inakua vigumu zaidi. Ila sijakata tamaa bado naendelea nao kuwafundisha maneno mawili matatu kila siku. Najitahidi sana kuwafundisha utamaduni wangu na mara kwa mara najitahidi pia kupika chakula cha kikwetu. Napenda sana chakula cha kitanzania na watoto wangu wanapenda sana nikipika chapati, maandazi, wali na maharage. Ukiwauliza wanapenda chakula gani cha kitanzania basi nina uhakika watakwambia chapati.

Amani (kushoto) na Malaika
                                                                   Amani (kushoto) na Malaika

Wewe binasfi unaamini majina ambayo wazazi wana wapa watoto wao yanachangia katika mafanikio yao kiuchumi, kielimu, na tabia zingine? Kwa mfano majina kama Amani anaweza akawa mtu wa kupenda amani siku zote, au majina kama Tabu, Sikujua yanaweza yaka changia mototo kuwa na matatizo katika maisha yake? Majina yanachangia sana katika maisha ya watoto wetu. Ndio maana mimi nilijitahidi sana kukaa na kufikiria majina ya kuwapa watoto wangu. Nimekua naamini hili kwa miaka mingi sana kuwa majina yana nguvu sana katika kujenga au kubomoa maisha ya muhusika. Huwa nashukuru sana kwa wazazi wangu kuamua kunipa jina la Zawadi nina imani kubwa hili jina limenisaidia kwa namna moja ua nyingine.

Kama mama mwenye watoto wenye asili mbili tofauti, ni changamoto gani unapata katika malezi yao, haswa katika maswala ya maadili, na utowaji wa adhabu pale mototo anapo kosea? Changamoto ni kubwa sana kwa kweli na hapa ndio unaweza kuona kuna utofauti mkubwa sana kati ya utamaduni zetu mbili. Nina imani waafrika wengi walioolewa na wazungu wanakumbana na ili tatizo. Mvutano wake ni mkubwa hasa kwenye maswala ya maadili na utoaji wa adhabu kila upande unaamini wenyewe ndio wanajua jinsi ya kulea zaidi.

Sisi tumeaumua kuchukua maadili mazuri toka pande zote mbili na kuacha mabaya. Ila bado wakati mwingine tunavutana maana watoto wanafurahia zaidi maadili ya wenzetu maana yako malaini na ya kudekeza sana. Mimi nachofanya ni kusimama na msimamo wangu wa kuunganisha mazuri toka pande zote mbili kwa namna hii nina imani tutafanikiwa kulea watoto wenye tabia nzuri na watakaua wamefaidika kutoka pande zote mbili.

Zawadi na familia yake
                                                                             Zawadi na familia yake

Unasafiri sana na mara zote huwa upo na familia yako yote (mmeo na watoto). Je nichangamato zipi huwa unapata maana nafikiri ni ngumu sana? Au huwa unakuwa na msaidizi (dada wa kazi)? Changamoto haziwezi kukosekana hasa ukiwa unasafiri na watoto wadogo. Ila faida zake ni kubwa ambapo hata hizo changamoto hazina nguvu tena. Mimi na mume wangu tunapenda kulea watoto wetu wenyewe kwa hiyo hatuna msaidizi wa watoto. Msaidizi tulie nae ni wa kusafisha nyumba tu ambae anakuja mara mbili kwa wiki. FB_IMG_1446686812537Ni ushauri gani ungependa kuwapa wakina mama ambao wanapenda kusafiri lakini wanaogopa kwa sababu ya watoto? Faida ya kusafiri na watoto ni kubwa kuliko matatizo. Sidhani kama mama ambae amezoea kulea watoto wake anaweza ogopa kusafiri nao. Hata unapokua safarini watoto unawalea kama ulivyozea kuwalea kinacho badilika ni mazingira tu ambapo kwa watoto ni rahisi sana kubadilika na kufuata mazingira waliyopo.

Tena unakuta wao ndio wanafurahi zaidi kuliko hata sisi wakubwa. Nawashauri wamama wenzangu tafadhali usiwaache watoto nyuma beba watoto wako nenda kawape kumbu kumbu na nafasi ya kujifunza mambo mapya yatawasaidia sana kwenye maisha yao ya baadae. Pia ni faida kubwa kwako mzazi maana ukiwa holiday unatumia muda wote kuwa pamoja na watoto wako na unajenga familia iliyokomaa na yenye kumbukumbu nzuri pia unawajengea watoto wako sifa ya kujiamini.

Unawezaje kumudu majukumu yako kama mama, mke, na kuendesha mambo ya kiuchumi ndani ya familia? Ni mgawanyiko unachagua kipi muhimu kwako kwanza. Mimi nimechagua kuwapa watoto wangu muda wangu zaidi kipindi hiki wakiwa wadogo kwa kuamua kua mama wa nyumbani ili nipate muda mzuri wa kuwalea. Kwa kukaa nyumbani napata muda wa kujihusisha na shughuli mbali mbali za maendeleo ya watoto wangu, na uamuzi huu umeniwezesha kujenga familia yangu na kuwa yenye furaha sana. Pia nipatapo muda najitahidi kujishughulisha na shughuli za kiuchumi za familia.

Zawadi, wewe ni mama ambaye unawatoto wawili lakini bado uko vizuri kabisa kama mdada ambaye hana watoto. Ni nini unafanya kujiweka katika hali hiyo? Hii ni changamoto kubwa nadhani sio kwangu tu ila kwa wamama wengi, hasa sisi tunaokua nyumbani unaweza kujisahau kabisa. Kwangu mimi changamoto niliyonayo ni mwili wangu ni rahisi sana kuongezeka kwa hiyo mara kwa mara lazima niwe kwenye diet na mazoezi maana bila hivyo naweza kuongezeka kupita kiasi, nikiongezeka nakosa raha kabisa maana napenda utanashati.

Nashukuru kwa namna hii inanisaidia kunikumbusha kuwa kuzaa isiwe sababu ya kuharibika na kwa sababu napenda kupendeza basi najikuta lazima nitafute muda wa kujipenda mimi. Weekend ni muda wangu mimi siku hizi mbili ni jukumu la mume kuangalia familia na mama huwa napumzika kabisa kama nikiamua kukaa nyumbani nawaachia mume na watoto wanilee mimi. Nikiamua kutoka basi utakuta naelekea shopping au spa au kutembelea marafiki, kwa staili hii najikuta napata muda wa kupumzika na kuwa na furaha muda wote.

Zawadi katika wedding Anniversary yake. Dubai-2014
                                          Zawadi katika wedding Anniversary yake. Dubai-2014

Siku hizi tunasoma kwenye blogs mbali mbali na kusikia baadhi ya wakina dada wa Kitanzania wana amini kuwa kuolewa na “mzungu” au mtu mwenye ngozi nyeupe ndio njia pekee ya kujikwamua si tuu kiuchumi bali hata kimapenzi. Je wewe unalionaje swala hili? Na nini ushauri wako kwa wadada hawa? Hili ni swali ni gumu kwa kweli ila nitajitahidi kujibu kwa mtazamo wangu ambao kwa kiasi kikubwa umechangia kwenye maisha yangu. Mimi binafsi naamini kuwa kuolewa na mzungu asilimia kubwa una nafasi ya kujikwamua kiuchumi pia kupata mapenzi ya dhati. Sisemi kama watu weupe pekee ndio wanaweza kukukwamua kiuchumi hata pia watu weusi. Ila kwenye mapenzi ya dhati nadhani kura zangu zote napeleka kwa wazungu. Wenzetu wanaheshimu mwanamke na akipenda amependa yuko tayari kufanya chochote kuonyesha upendo wake. Hapo ndio tunakuja kwenye suala la uchumi mzungu akikupenda yuko tayari kukufanyia chochote kile utakacho, anachojali yeye ni furaha yako.

Ushauri wangu ni kwamba kila kitu kina pande mbili nzuri na mbaya. Wazungu pia nao ni binadamu kama binadamu wengine wana mabaya na mazuri yao. Nawashauri kabla hawajajitumbukiza kwenye maisha ya hawa watu kwanza wachunguze je watawezana nao hasa kwenye upande wa pili ambao si mzuri? Maana naona wengi wanaangalia upande mmoja tu ambao ni mzuri. Inachukua muda mrefu kwa wazungu kutuamini sisi Waafrika maana wengi wanaamini kuwa Waafrika hatuna mapenzi ya kweli na wengi wetu ni waongo sana na hakuna kitu ambacho mzungu anachukia kama uongo.

Zawadi na mumewe
                                                              Zawadi na mumewe

Hata kama anakupenda kiasi gani akishagundua tu kuwa wewe una vitabia vya uongo lazima atakukimbia tu. Kwa hiyo ushauri wangu mwingine kwa kina dada ambao wanapenda kuolewa na hawa watu kuwa wakweli kuanzia mwanzo, hata kama una vitabia vibaya wewe usijali mzungu akikupenda amekupenda yuko tayari kukusaidia kubadilisha hivyo vitabia au hata kuvumilia kuishi navyo maana wenzetu wana mapenzi ya dhani na ikitokea kama hatoweza au ajapendezwa na hivyo vitabia basi atakwambia ukweli mapema. Asilimia kubwa ya wazungu akikupenda amekupenda na yuko tayari kusimama kwa ajili yako kwa jambo lolote ila lazima uwe mkweli. Kwa kina dada wote ambao ndoto zao ni za kuolewa na hawa wenzetu mimi nasema usikubali mtu yoyote akukatishe tamaa, endeleza ndoto yako maana faida yake ni kubwa kuliko hasara.

Marehemu mama yake Zawadi.....R.I.P
                                                      Marehemu mama yake Zawadi…..R.I.P

Zawadi, wewe ni dada ambaye mzazi wako mmoja (mama mzazi) hayupo nawe tena. Uliwezaje kupata nguvu ya kuendela na maisha bila kukata tamaa, maana kuna watu wengi ambao wameshindwa kuendelea au kukata tama ya maisha baadaya ya kuondokewa na mzazi au wazazi wao? Kwa kweli nimepitia matatizo mengi sana namshukuru Mungu hakuweza kunitupa alinilinda na kufanikiwa kuvuka vikwazo vingi sana katika maisha yangu. Usiombe ufiwe na mama hasa ukiwa na umri mdogo maana nguzo kubwa ya familia Afrika ni mama. Mimi nilipoteza mama nikiwa na miaka kumi na tano huku nikiwa na wadogo ambao walikua wadogo zaidi, mdogo wangu wa mwisho aliachwa akiwa na miezi kumi tu. Kusema kweli nimepitia kipindi kigumu sana mapaka kufikia hapa nilipo ila namshukuru mwenyezi Mungu hakuweza kunitupa.

Zawadi na mdogo wake aitwaye Tina
                                         Zawadi na mdogo wake aitwaye Tina

Hili swali hili huwa linanipa wakati mgumu sana maana kumbu kumbu zote huwa zinarudi mtanisamehe kama nitakua nimejibu kwa kupitiliza maana kuna mengi sana ila nitajitahidi kujibu kwa ufupi zaidi. Hakuna kitu kibaya hapa duniani kama dharau, usimdharau mtu hata siku moja maana uwezi jua huyo mtu siku moja atakua wapi. Pale mama alivyofariki tu ndio tulianza kujua rangi halisi ya ndugu zetu na zinasikitisha kwa kweli.

Namshukuru Mungu alinipa ujasilia wa hali ya juu na kuweza kusimama na kusaidia wadogo zangu pia. Ilibidi nikue kwa kasi ya ajabu ili niweze kuwasaidia wenzangu ambapo kwenye umri wa usichana badala ya kufurahia maisha mimi nilikua najiuliza nitawalishaje wadogo zangu, vipi wana nguo za kuvaa, je school fees safari hii nitaipata wapi. Kwa namna hii sikuweza kupata bahati ya kuendelea na elimu ya juu na kuamua kutafuta kozi fupi fupi ambayo ingeniwezesha kumaliza mapema na kupata ajira ili niweze kupata mshahara ili niweze kuwasaidia wadogo zangu. Na kwa bahati mbaya mpaka leo bado sijaweza kukamilisha hii ndoto ya kupata elimu ya juu ila bado naamini kuwa kila kitu na wakati muda muafaka utafika ambapo kutakua hakuna kipingamizi kitakachosimama kati yangu na ndoto yangu ya mwisho. Nina imani lazima nitalikamilisha sababu ni kitu ambacho napenda. FB_IMG_1446692135293-1Mimi ni mpiganaji na ambae sikati tamaa kirahisi na hiki ndicho kimenisaidia kufika hapa nilipo. Nilikua najua nataka nini na sikuacha kutafuta nachokitaka. Nilipitia vizingiti vingi lakini havikunikatisha tamaa kabisa na pale nilipoona karibu naanza kukata tamaa nilisali sana maana mwenyeji Mungu pekee ndio alikua anaujua moyo wangu, kwa asilimia mia nilikua nina uhakika siku moja atanisaidia tu na kunipa maisha ambayo nayataka, imani hii iliendelea kunipa nguvu kwa kiasi kikubwa sana.

Kitu kingine ambacho kilinisaidia ni kuthamini watu wa aina yote, nilijitahidi kuwa na upendo kwa watu wote, kwa namna hii iliniwezesha kuishi na watu wa aina tofuati ambao wengi walinisaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha maisha yangu. Yaani siwezi kuwasahau watu wote ambao walinisaidia kipindi hicho wengi ni watu baki ambao hatuna uhusiano wowote. Kitu ambacho hawakuja ni kwamba msaada wao ulikua ni mkubwa sana kwangu.

Nachofanya siku hizi kila nipatapo nafasi ya kukutana na hao watu nawakumbusha na kuwashukuru ambao karibu wote wameshasahau hata kama waliwahi nisaidia nini. Kutokana na msaada wao walionipa enzi hizo umenifanya hata mimi pia kuwa na tabia ya kupenda kusaidia watu wa aina tofauti bila kujali wanatokea kwenye mazingira ya namna gani. Pia huwa najitahidi kusaidia pale ninapoombwa msaada hasa kwa watu ambao nina uhakika msaada wangu utawasaidia kwa kiasi kikubwa.

Huwa naamini msaada ni msaada hata uwe mdogo kiasi gani kwenye macho yako lakini kwa anayesaidiwa ni kitu kikubwa sana kwake. Nakumbuka kuna siku nilisaidiwa na mtu nauli tu ya daladala ya kwenda kazini hapo nilikua sina pesa hata ya nauli ya kwenda kazini. Msaada wake uliweza nifikisha ofisini na hapo niliweza pata pesa ambazo ziliweza kusaidia kupata chakula cha wadogo zangu siku inayofuata pia nauli yao ya kwenda na kurudi tution. 2015-11-05 07.25.45Mtu gani ambaye wewe unamuangalia kama kioo chako (your role model), na kwanini? Huwa navutiwa sana na watu ambao wana moyo wa kusaidia wengine kwa namna moja au nyingine. Na Oprah ana sifa hiyo kubwa. Nimejikuta najifunza, nacheka, nasikitika, nalia na hata kupata nguvu mpya kipindi chote nilichokua naangalia show zake.

Pia nimejifunza mengi kutoka kwenye magazeti yake kwa miaka mingi nimekua msomaji wake mkubwa. Napenda karibu kila kitu kuhusu Oprah kasoro kwenye suala la mbwa tu lol! Mimi ni mmoja wa wale watu wanaoamini kuwa mnyama ni mnyama na alelewe kama mnyama na sio kama binadamu, mtanisamehe kwa wale ambao nime wakwaza naelewa maana mume na watoto wangu hawakubaliani nami kwa suala hili.

Zawadi Kakoschke Blogger was www.maisafari.com
                                Zawadi Kakoschke Blogger wa www.maisafari.com

Ujumbe au ushauri wowote kwa wamama wenzako: Tupendane! Hakuna kitu kizuri maishani kama upendo maana upendo unajenga heshima, furaha, amani na mengine mengi. Sisi kama kina mama tunajukumu la kulea watoto wetu ambao baadae wataongoza taifa letu. Sasa kama sisi kina mama hatutakua na upendo ina maana tunawajengea watoto wetu taifa ambalo litakua na majanga huko mbeleni.

Ushauri au ujumbe kwa wadada au wanawake ambao hawajaolewa na wangependa kuolewa: Kwanza kabisa jiheshimu na jitambue wewe ni nani na unataka nini. Baada ya hapo mtangulize Mungu mbele ili aweze kukuchagulia mume mwenye upendo. Ila usiache kutafuta kile unachotaka hata Mungu nae anakubali kubembelezwa hasa pale anatakapokua amekuletea mume ambae humtaki ni ruksa kuomba kubadilishiwa.

Mimi pia nilimbembeleza Mungu anitafutie mume mwema mwenye upendo ila sikuacha kuweka kwenye sala zangu na kusema tafadhali naomba awe mzungu maana nilikua najijua nisingeweza kuwa na furaha ya ndoa kama angeniletea mume wa kutoka kwetu. Ingawa wanasema kuwa si vizuri kumchagulia Mungu yeye anajua zaidi, lakini pia Mungu ni mwenye upendo wa dhati angependa kukuona ukiwa na furaha. Kwa hiyo wapendwa usiache kumbembeleza ili aweze kukupa kile unachotaka. Kwangu mimi kanipa kile nilichoomba kabisa kwa kweli mwenyezi Mungu yupo na anasikiliza maombi yetu siku zote.

Na mwisho, ujumbe kwa Watanzania wenzako: Tuache tabia ya kupenda kuhukumu watu hasa tusio wajua na tuache chuki zisizo na msingi. Utakuta mtu hata hakujui lakini utakuta ameshakupa hukumu ya hatari utadhani anakujua, hiyo yote ni chuki ambayo ni mbaya sana. Tupendane jamani upendo ni kitu cha bure na chenye mafanikio makubwa.

Asante sana Zawadi.

Source: Mahojiano haya yamefanywa na Alpha Igogo

2 thoughts on “Mahojiano maalum: Zawadi Kakoschke”

Leave a Reply